Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi

Eliezer Mbuki Feleshi photo
Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi
Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Barua pepe: info@agctz.go.tz

Simu:

Wasifu

NYUMBANI NA FAMILIA

Mheshimiwa Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi alizaliwa tarehe 1 Julai, 1967 na kukulia katika Kijiji cha Malya, Kwimba mkoani Mwanza, Tanzania. Ameoa mwaka 1994 na amejaliwa kupata watoto wanne. Yeye ni kitindamimba kati ya watoto tisa kwenye familia ya Kikristo.

ELIMU NA MAFUNZO

Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi alijiunga na Shule ya Msingi Malya mwaka 1976 na kumaliza mwaka 1982. Aliendelea na Elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari Shinyanga mwaka 1983 hadi 1986 na baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Galanos kwa ajili ya masomo ya Kidato cha Tano na Sita kuanzia mwaka 1987 hadi 1989.

Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi alipata Shahada ya Kwanza ya Sheria (LLB)(Hons) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1994. Baada ya hapo, alihitimu Shahada ya Uzamili ya Sheria (LLM) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2005 akizamia katika Sheria ya Jinai, Mwenendo wa Makosa ya Jinai na Utoaji Adhabu. Mwaka 2011 alitunukiwa Shahada ya Uzamivu (Sheria) katika Jinai na Utoaji Adhabu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

HISTORIA YAKE SERIKALINI

Kabla ya kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 12 Septemba, 2021, Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi alikuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo alitumikia nafasi hiyo kuanzia tarehe 2 Juni, 2018. Kama Jaji Kiongozi, Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi alishiriki kikamilifu na kwa ufanisi katika usimamizi wa Mahakama na maboresho yaliyoongozwa na Mahakama chini ya uongozi wa Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania na alifanya kazi kwa karibu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Msajili Mkuu wa Mahakama na wajumbe wengine waandamizi wa Mahakama katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama wa 2015/16–2019/20 kuelekea Utoaji wa Huduma za Haki Unaowazingatia Wananchi. Aidha, alishiriki kufanyia kazi Mpango Mkakati wa sasa wa Mahakama wa 2020/21–2024/25.

Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi alikuwa pia Jaji wa Mahakama Kuu kuanzia Agosti, 2014 hadi Septemba, 2021 ambapo alifanya kazi katika kituo cha Dar es Salaam kuanzia Agosti, 2014 hadi Februari, 2017; Masjala ya Iringa kuanzia Februari, 2017 hadi Juni, 2018 na Masjala Kuu kuanzia Juni, 2018 hadi Septemba, 2021.

Akiwa Jaji Kiongozi na Jaji wa Mahakama Kuu, Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi aliongoza Masjala Kuu ya Mahakama Kuu ya Tanzania na kushiriki katika utoaji maamuzi ya mashauri, pia, alishiriki katika usimamizi wa usikilizwaji na utoaji wa uamuzi ya mashauri mbalimbali ya Mahakama Kuu, Mahakama za Wilaya, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Mwanzo nchini. Katika kipindi hicho, Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi aliamua idadi kubwa ya mashauri yanayohusiana na madai ya Katiba, uchaguzi, ardhi, biashara, uasili na ndoa. Aidha, aliamua idadi kubwa ya mashauri yanazohusiana na jinai kwa mashauri yanayohusiana na uhujumu uchumi na rushwa. Vilevile, Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi alifanikiwa kufanya mapitio ya mashauri mbalimbali za jinai na madai na alihakikisha mashauri yanamalizika kwa wakati na idadi ya mashauri yaliyofunguliwa kila mwaka inakuwa juu kuliko mashauri yanazosubiri kuamuliwa.

Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi aliongoza Baraza la Elimu ya Sheria katika mchakato wa kupitia na kuchambua kidijitali maombi ya kupokelewa na kuandikishwa kuwa mawakili wa kujitegemea yaliyowasilishwa na wahitimu wa Shahada ya Sheria. Aidha, aliandaa miongozo ya ukaguzi kwa kampuni za kisheria na shule au vitivo vya sheria.

Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi pia alihudumu kama Mkurugenzi wa Mashtaka kuanzia Machi, 2007 hadi Agosti, 2014. Akiwa Mkurugenzi wa Mashtaka, Jaji Dkt. Feleshi alishiriki katika maboresho ya haki jinai hususan katika uendeshaji wa upelelezi wa makosa ya jinai na uendeshaji wa mashtaka wakati na baada ya kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka mwaka 2018. Sheria ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Sura ya 430 ilipoanza kutumika, Ofisi yake ilizindua mabadiliko ya uendeshaji wa huduma ya mashtaka na uratibu wa uchunguzi wa mashauri makubwa chini ya Mpango wa Uchunguzi Unaoongozwa na Uendeshaji Mashtaka. Mashauri yanayotumia Mpango huo ni pamoja na yale yanayohusiana na EPA (BOT External Payment Arears Scam), mpango wa piramidi unaojulikana kama “Development for Entrepreneurship Community Initiative (DECI)” ugaidi, mauaji ya watu wenye ualbino na makosa ya ujangili, kwa kutaja machache.

Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi alitumia kwa ufanisi Jukwaa la Kitaifa la Haki Jinai ili kutatua changamoto zinazokabili taasisi za haki jinai. Aidha, alitumia Tangazo la Serikali Na. 296 la mwaka 2012 kama mwongozo sahihi wa kufungua na kuendesha mashauri ya Jinai hatua iliyochangia kuondoa msongamano wa wafungwa magerezani. Kutokana na hali hiyo, wastani wa msongamano wa wafungwa ulipungua kutoka wafungwa 47,000 kwa siku mwaka 2006/2007 hadi wafungwa 32,000 kwa siku kwa kipindi cha mwezi Agosti, 2014 kinyume na uwezo ulioidhinishwa wa malazi wa wakati huo ambao ulikuwa wafungwa 29,552 kwa wakati mmoja.

Akiwa Mkurugenzi wa Mashtaka na Mratibu wa Programu ya Mafunzo kwa Wahitimu wa Shahada Sheria wakati huo, Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Mikakati mwaka 2008 ambayo iliandaa Mtaala na Kanuni za Shule ya Sheria Tanzania kwa kuzingatia Sheria ya Shule ya Sheria Tanzania, Sura ya 425, hati zilizofungua njia ya uzinduzi na uendeshaji wa Shule ya Sheria ya Tanzania chini ya Bodi ya Uongozi ya Shule ya Sheria Tanzania katika mwaka huo huo.

Kuanzia mwaka 2008 hadi 2014, Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi alifanya kazi na Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika (APA) na Chama cha Kimataifa cha Waendesha Mashtaka (IAP) na alishiriki katika kuanzisha Mtandao wa Wakala wa Urejeshaji Mali Kusini mwa Afrika (ARINSA) mwaka 2009 na Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika Mashariki (EAAP) mwaka 2010. Katika muktadha huo, alihudumu kama Makamu wa Rais na Mshauri Mkuu wa APA na EAAP mtawalia.

Kwa kuzingatia umahiri alionao katika taaluma yake, Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi kwa nyakati tofauti alipokea na kutoa huduma za ushauri kwa mashirika ya kitaifa na kimataifa katika kuzuia na kudhibiti uhalifu wa kimataifa hususan ugaidi, rushwa, dawa za kulevya na usafirishaji haramu wa binadamu, uhalifu wa kifedha, uharamia wa baharini na urejeshaji wa mali zilizoibiwa. Mashirika hayo ya kimataifa yalijumuisha Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (ISS), Mtandao wa Wakala wa Urejeshaji Mali wa Kusini mwa Afrika (ARINSA), Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC); Urejeshaji wa Mali Iliyoibiwa (Mipango ya Nyota) na Kitengo cha Sheria na Mambo ya Kikatiba cha Jumuiya ya Madola.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka tarehe 26 Machi, 2007, Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi alihudumu kwa muda wa miaka kumi na mbili (12) kama Wakili wa Serikali katika madaraja tofauti na hatimaye aliteuliwa kuwa Wakili wa Serikali Mfawidhi wa Kanda ambapo, miongoni mwa majukumu mengine, aliendesha mashtaka na mashauri makubwa na rufaa katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Aidha, amekuwa akishiriki katika timu za uchunguzi zilizoundwa na Mamlaka za Juu. Mathalani, mwaka 2006 alihudumu kama Katibu wa Tume ya Kipenka ambayo ilikuwa Tume ya Rais iliyoundwa kuchunguza mauaji ya wafanyabiashara wanne wa madini kutoka Mahenge Ulanga Morogoro yaliyotokea eneo la Palestina, Sinza Jijini Dar es Salaam. Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi pia amewahi kuhudumu kama Katibu wa Kamati ya Mawaziri iliyoundwa kuchunguza migogoro ya kimkataba ya ujenzi wa Barabara ya Kitaifa na madai yaliyohusisha Serikali na kampuni tatu za kigeni za ujenzi wa barabara ambazo ni M/S KARAFI International, M/S, Konoike Construction Co. Ltd na M. /S SIETCO.

MAJUKUMU MENGINE NA TEUZI

Kwa sasa, Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi anahudumu katika nyadhifa mbalimbali ikijumuisha kuwa Mjumbe wa Tume ya Huduma za Mahakama kuanzia Juni, 2018; Mwenyekiti wa Wasuluhishi, Wapatanishi na Washiriki wa Jopo la Ithibati (kuanzia Septemba, 2021); Mwenyekiti wa Timu ya Sheria ya Serikali (kuanzia Septemba, 2021) na Mjumbe wa Kamati ya Taifa ya Uongozi ya Uwekezaji (kuanzia Septemba, 2021). Aidha, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili kwa Maafisa Sheria ya Baraza la Elimu ya Sheria kuanzia Juni, 2018 hadi Septemba, 2021 Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Majaji kuanzia Februari, 2017 hadi Juni, 2018; Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kuanzia Septemba 2016 hadi Septemba, 2021. Pia amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadilii ya Madalali wa Mahakama na Michakato ya Mahakama ya Uteuzi, Mishahara na Nidhamu kuanzia Juni, 2018 hadi Septemba, 2021, vile vile, amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mawakili kuanzia Septemba, 2015 hadi Juni, 2018. Mwisho lakini sio kwa umuhimu wake, Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi amekuwa Makamu wa Rais wa APA kwa vipindi viwili na mwanzilishi na Mshauri Mkuu wa kwanza na baadaye Makamu wa Rais wa Chama cha Waendesha Mashtaka wa Afrika Mashariki.

MAJUKUMU NA MCHANGO WAKE KATIKA SEKTA YA SHERIA

Katika kuendeleza kazi kubwa iliyofanywa na watangulizi wake tisa, Mhe. Jaji Dkt. Feleshi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mlezi wa Chama cha Wanasheria wa Serikali, tangu tarehe 13 Septemba, 2021 hadi leo ameendelea kutekeleza majukumu mahsusi na ya jumla katika kusimamia Maafisa Sheria  na Mawakili wa Serikali takriban 3,355. Amekuwa akiyatekeleza hayo kwa msaada wa Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Menejimenti ya OMMS) na Timu ya Sheria ya Serikali (GLT) inayoundwa na  Mkurugenziwa wa Mashtaka, Wakili Mkuu wa Serikali, Kabidhi Wasii Mkuu, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Mwandishi Mkuu wa Sheria na Wakurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Wizara za Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya Rais–Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika kuendeleza na kuboresha huduma za kisheria ambacpo katika Mapinduzi ya 4 ya Viwanda Duniani, OMMS  imepiga hatua kubwa na kupata matokeo mazuri.

Kutokana na matokeo hayo, tarehe 16 Septemba, 2021 Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi alipata kibali cha Serikali cha kuanzisha Programu ya Vituo Jumuishi vya  Taasisi za Kisheria za Serikali inayotambulika kama GLIICs ili kwenda sambamba na Vituo Jumuishi vya Haki vya Mahakama, yaani IJCs ili kuwezesha utoaji wa huduma za haki kutoka kwa OMMS, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, OWM na taasisi nyingine za kisheria ziweze kupatikana na kutolewa kwa umma na wadau wengine katika sehemu moja. Ujenzi wa jengo la kwanza chini ya Programu ya GLIICs ulizinduliwa mnamo mwezi Novemba, 2022 katika eneo la Buswelu Mwanza na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro.

Hatua nyingine ya kimkakati iliyofuatia ni kuanzishwa kwa Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (oagmiss-http://oagmiss.agctz.go.tz) na kuboreshwa kwa mfumo wa OAG e-Office. Hatua hizi zilitekelezwa kuanzia mwezi Septemba, 2021 hadi Septemba, 2022 zikienda sambamba na ugawaji wa vifaa vya kisasa vya kielektroniki  kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa madhumuni ya kukuza na kuendeleza uwezo wao katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Uzinduzi wa mfumo wa oagmiss, nembo ya OMM, Chama cha Wanasheria wa Serikali pamoja Daftari la Orodha ya Mawakili wa Serikali ulifanywa na Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 29 Septemba, 2022. Aidha, mfumo unaotoa fursa ya haraka na rahisi kwa watumiaji kujiunga na kutumia Orodha ya Mawakili wa Serikali kimtandao, tovuti ya OAG, ukurusa wa tovuti ya OMMS Mrejesho na Katalogi ya Sheria Mtandao iiliyopakia sheria kuu zilizotungwa na Bunge.

Katika kipindi hiki, Divisheni ya Uandishi wa Sheria imebadilishwa muundo wake na kuwa Ofisi huru ndani ya OMMS ili kuimarisha huduma zake za Uandishi, Urekebu na Ufasiri wa Sheria. Mageuzi haya yana lengo la kufanikisha kuchapisha na kutangaza Toleo la Urekebu la Mwaka 2023 mapema mwaka 2024 litakalojumuisha Sheria Kuu 446 na Sheria Ndogo 1,439 pamoja na Fahirisi yake. Aidha, itajumuisha kutangaza Orodha ya Majina ya Sheria Kuu (ambayo yatatumika katika lugha ya Kiswahili ili kuondoa mkanganyiko katika matumizi ya Kiswahili). Kutafsiri Sheria Kuu na Sheria Ndogo zote kutoka lugha ya Kiingereza kwenda katika lugha ya Kiswahili na vinginevyo, pamoja na kutengeneza Istilahi za Kisheria katika lugha ya Kiswahili. Vile vile, itajumuisha kutoa Mwongozo wa Uandishi wa Sheria Toleo la Mwaka 2023 na Mwongozo  Maalum wa Uandishi wa Sheria Ndogo wa wizara, idara na serikali za mitaa kwa matumizi ya OMMS, Bunge, Mahakama, taasisi za elimu na wadau wengine.

Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi na Menejimenti ya OMMS wanatumia kila fursa inayopatikana kubainisha upungufu wa ujuzi na ustadi kwa wanasheria wapya na waandamizi, lengo likiwa ni kuwajengea na kuimarisha uwezo wao katika kushughulikia majadiliano ya aina mbalimbali pamoja na upekuzi na uhakiki wa makubaliano na mikataba. Makubaliano ya kifedha yanayohusiana na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, benki binafsi, dhamana za serikali na mikataba ya huduma na uwekezaji inayosaidiwa na mifumo ya kisheria na kitaasisi imebainisha umuhimu mkubwa wa kuwa na mawakili wa serikali mahiri na weledi ambao katika utekelezaji wa majukumu yao wanapaswa kuzingatia thamani ya fedha na kulinda maslahi ya umma. Ushiriki wao katika miradi mikubwa kama Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki maarufu kama EACOP, ununuzi wa ndege za Serikali, Ujenzi wa barababara za juu za kimkakati Jijini Dar es Salaam,  skimu za umwagiliaji maji, Mradi wa Reli ya SGR, ujenzi wa Bwawa la Uzalishaji Umeme la Mwalimu Nyerere yaani JNHPP, Gesi Asili ya LNG na Mradi wa DP World ambao uko katika majadiliano, imesaidia kubainisha umuhimu mkubwa wa kuwa na mafunzo endelevu na tafiti katika maeneo hayo, jambo lililoilazimisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuchukua hatua stahiki ambapo mwezi Novemba, 2023 imeandaa na kutoa Mwongozo wa Usimamizi wa Mikataba kwa matumizi ya Mawakili wa Serikali, wahadhiri na wadau wengine.

Ni kutokana na hali hiyo hapo juu, hatua stahiki zaidi zinachukuliwa kuhakikisha OMMS inakuwa na watumishi wa kutosha, vitendea kazi bora na stahiki pamoja na rasilimali nyingine muhimu. Hatua mbalimbali zilizochuliwa na watangulizi wa Mhe. Jaji Dkt. Feleshi na kuziendeleza katika maeneo hayo zinazojumuisha utendaji kazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu katika kipindi cha miaka mitano (1 Julai, 2018 hadi 15 Juni, 2023), zimeokoa mabilioni ya Dola za Kimarekani na Shilingi za Kitanzania katika utatuzi wa migogoro kama ilivyotolewa taarifa katika Mikutano ya Bunge husika.

Agenda ya maeguzi ya Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi  na Menejimenti ya OMMS kupitia ujenzi na uimarishaji wa mfumo wa utendaji kazi inasaidiwa na madawati mbalimbali yaliyoanzishwa mwaka 2022 ndani ya OMMS kwa ajili ya kushughulikia masuala mahsusi. Madawati hayo yanajumuisha Dawati la Ushirikiano baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano na ile ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mbali na hilo, kuna Namba ya Bure ya kuwasilisha na kupokea malalamiko na kutoa ushauri wa kisheria wa haraka kwa umma na wadau wengine ambayo inalisaidia jukwaa la kitovuti la oagmiss au https://www.agctz.go.tz. Hata hivyo, ili kuhakikisha uwepo wa maadili ya kitaaaluma miongoni mwa mawakili katika ofisi za sheria za umma, OMMS imezindua mwongozo wa masuala ya kimaadili dhidi ya Mawakili wa Serikali wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao unaoitwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Utekelezaji wa Majukumu) Mwongozo wa Utoaji Ushauri wa Kisheria kwa Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria uliyotangazwa katika Gazeti la Serikali la mwezi Januari, 2023. Pamoja na mafanikio hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali anasonga mbele akisisitiza kuwa “KAZI INAENDELEA”.

UANACHAMA WA KITAALUMA

Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi ni Mwanachama Binafsi wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Jumuiya ya Madola (mwenye Namba ya Uanachama: 0123); Mjumbe wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT); Mwanachama wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika asiyefanya kazi za uwakili binafsi (mwenye Namba ya Uanachama (TLS- Roll No. 2924) na ni Mwanachama Binafsi wa Chama cha Kimataifa cha Waendesha Mashtaka (mwenye Namba ya Uanachama (IAP 186717039).

MAMBO ANAYOYAPENDA

Mheshimiwa Jaji Dkt. Feleshi anapenda kusikiliza muziki wa injili pamoja na kutambua na kufanya utafiti na uchunguzi katika maeneo mbalimbali na ya kimkakati. Aidha, anapenda kusafiri, kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mipango mkakati iliyoidhinishwa.

______________________________