BAJETI YA KUTOSHA ITATUWEZESHA KUTEKELEZA MAJUKUMU KWA WAKATI-AG FELESHI

Imewekwa: 24 Oct, 2022
BAJETI YA KUTOSHA ITATUWEZESHA  KUTEKELEZA MAJUKUMU KWA WAKATI-AG FELESHI

BAJETI YA KUTOSHA ITATUWEZESHA  KUTEKELEZA MAJUKUMU KWA WAKATI-AG FELESHI

Na Mwandishi wetu

Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Mhe. Jaji Dkt Eliezer  Feleshi ameelezea  haja na umuhimu wa Ofisi  kuwa na  bajeti  ya kutosha  itakayoiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa tija, weledi na kwa wakati.

Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipoitembelea   timu   ya wataalamu  inayopitia miongozo iliyoandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Timu hiyo na ambayo ipo chini ya  Jaji Mstaafu Juxon Mlay inaendelea na   jukumu  hilo katika ukumbi wa  Mikutano wa Mahakama ya Kisutu  Mkoani Dar es Salaam

Mwanasheria Mkuu  amewaeleza wataalamu hao  kwamba,  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ikiwa na bajeti ya kutosha itakuwa huru na itakuwa  na uwezo mkubwa wa kuboresha  maeneo mengi likiwamo eneo la kufanya  tafiti  zinazohusu masuala ya sheria, makubaliano ya kimataifa na kufanyia kazi maeneo mengine bila  kusubiri  maelekezo kutoka Serikalini.   

“Tukiwa na  bajeti ya kutosha itakuwa rahisi kwetu kufanya mambo mengi na kwa wakati, kwa mfano,  tunaweza kufanya tafiti zinazohusu masuala ya  sheria na hata kwa kazi  za kuandika sheria  na kutafsiri  sheria  kwa lugha ya  Kiswahili  tutaweza kuzifanya kwa wakati”. Akasema  

  Na kuongeza“ Matumini na hamu yangu  kubwa ni kwa Ofisi hii kuwa na bajeti inayojitosheleza”

Pamoja na  kuelezea hamu  kubwa ya kutaka  Ofisi iwe na Bajeti ya kutosha, Mwanasheria Mkuu Feleshi pia ameelezea kuridhishwa kwake na  kazi inayofanywa na wataalamu hao  ya kupitia  miongozo hiyo.

“ Nitoe shukrani zangu za dhati kwenu, kwanza, kwa kukubali kwenu kuja kupitia na kutoa mawazo yenu ya kitaalamu kwenye miongozo hii ambayo . Nimeridhishwa na kufurahishwa na maendeleo ya kazi hii na ni matumaini yangu itakamilika kwa wakati

Akasisitiza  kuwa  maoni  yaliyotolewa na  wataalamu hao kuhusu   miongozo hiyo ameyapokea na yataendelea kufanyiwa kazi.

 

Kwa  upande wao wakiongea kwa nyakati  tofauti,  Watalaamu hao   wameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kwa kuaandaa miongozo hiyo  na kwa wao kupewa heshima ya kuifanyia kazi na kutoa mawazo yao.

Akitoa  maoni yake,  Jaji Mstaafu Juxon Mlay alikuwa na haya ya kusema “ Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali , sisi tunashukuru kwa kutukumbuka na kuona kwamba  tunafaa kuipitia  miongozo hii na kutoa maoni yetu ya kitaalamu”.

Akaeleza  zaidi  kwa kusema. “Tunashukuru pia  kwa kuipitia miongozi hii tumepata  fursa yakujikumbusha kwani nasi  tuliwahi  kufanya kazi  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika nafasi mbalimbali, tumekutana   tena na kukaa pamoja kuifanya kazi  hii na kutoa mawazo yetu ni  fursa  na tunajisikia kuthaminiwa”.

Baadhi ya  mapendekezo ya jumla waliyowasilisha ni pamoja na  kutaka   miongozo itoe maelekezo ya hatua kwa hatua yatakayomsaidia   Wakili wa Serikali popote alipo kutekeleza   majukumu yake kwa weledi  na maarifa.

Aidha wameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kwa kuandaa miongozo hiyo ikiwa ni  pamoja na kuanzisha Chama  cha Mawakili wa Serikali.

Pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kuitembelea  timu hiyo,  Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali   Dkt. Evaristo Longopa na  Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole nao walipata nafasi ya kuitembelea timu  hiyo na kuzungumza nao.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Jaji Feleshi aliunda timu ya wataalamu inayohusisha mawakili wa serikali waandamizi kwaajili ya kuipitia na kuiboresha miongozo ambayo imeandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kabla miongozo hiyo haijaanza  kutumika.

Wataalamu   hao  ni  Jaji Mstaafu Juxon Mlay ambaye amewahi kuwa  Naibu Mwandishi Mkuu wa Sheria na Mkurugenzi wa Mashtaka,    Jaji mstaafu  Julius  Malaba aliyewahi pia  kuwa  Mkurugenzi wa Divisheni  ya Mikataba , Jaji mstaafu  S. Bentram Matupa ambaye amewahi kuwa Katibu wa Mwanasheria Mkuu  wa Serikali  na Bi. Sarah Barahomoka aliyewahi kuwa Mwandishi Mkuu wa Sheria.

Pia wapo  Mawakili wa Serikali  waandamizi  kutoka Divisheni ya Uandishi wa  Sheria, Divisheni ya Mikataba na  Divisheni  ya Uratibu na Ushauri wa Kisheria.