FANYENI KAZI MSISUBIRI VYEO - AG FELESHI

Imewekwa: 17 Nov, 2022
FANYENI  KAZI  MSISUBIRI VYEO  -  AG FELESHI

Na Mwandishi Maalum

Dodoma

17/11/2022

 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali   Mhe. Jaji Dkt. Eliezer  Mbuki Feleshi amerejea wito wake  wa   kuwataka   Watumishi  waliopo katika  Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  na Wakili  Mkuu wa Serikali  kutekeleza  majumuku yao  kwa weledi , uaminifu na uadilifu  na siyo kusubiri teuzi au vyeo.

Ametoa rai hiyo leo,  alhamisi  wakati   wa mazungumzo yake  na Wakili  Mkuu wa Serikali  Dkt Bonifance Luhende na  Naibu Wakili  Mkuu  Bi. Sara Mwaipopo   waliofika Ofisini kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali   katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Katika  mazungumzo hayo na ambayo pia yalihudhuriwa na  Menejimenti,  Mawakili Wakuu  na Mawakili  wa  Waandamizi wote kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Dkt. Feleshi amesema,   uongozi  hautafutwi ,uongozi unakuja kwa kufanya kazi.

“ Niwapongeze kwa kuaminiwa  na  kuteuliwa kwenu na Mhe. Rais kushika nafasi hizo za uongozi. Uongozi   hautafutwi,  tekeleza majukumu yako, jukumu  ulilonalo mkononi ndilo lako, timiza wajibu wako na mengine yatafuata”. Amesisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  amesisitiza haja na umuhimu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali  kuwa na  ushirikiano wa karibu  na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake ambayo  kimsingi  Ofisi hiyo inatekeleza kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali .

Akielezea Zaidi kuhuhusu haja na umuhimu wa Ofisi hizo mbili  wa kufanya kazi kwa Karibu,  Mwanasheria Mkuu wa Serikali amebainisha kuwa taratibu  kadhaa zimeshawekwa zikiwamo za kuwa na  maafisa dawati wanaoratibu   mawasiliano na ubadilishanaji wa taarifa kwa haraka na kwa wakati baina ya  Ofisi hizo   mbili.

 Naye   Wakili Mkuu  Mkuu wa Serikali  Dkt. Bonifance  Luhende amemhakikishia Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kwamba, yeye binafsi, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali  na Ofisi yote wanalichukulia suala na   uhusiano na Ushirikiano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa ni jambo  la kipaumbele.

Dkt Lunhede  amesema,   Ofisi hizo mbili  ni  kiungo  muhimu  katika kuisadia Serikali   kufikia malengo yake  yakiwamo ya kuwaleta wananchi  maendeleo,  lakini  pia ni Ofisi  ambazo  mambo mengi na mazito  yanapita kwenye Ofisi hizo, mambo ambayo  wakati mwingine yanahitaji ushauri wa haraka au maamuzi ya haraka hivyo ushirikiano na mawasiliano   kati yake  ni jambo ambalo  halikwepeki.

“Ofisi zetu hizi zina mambo mazito  yanayopita mikononi mwetu, mambo  yanayohitaji    wakati mwingine   kutoa ushauri na maamuzi ya  haraka  kwa Serikali ili mambo  yaweze Kwenda.   Kwa hiyo  kwetu sisi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali  jambo la ushirikiano na Ofisi yako, Mhe  Mwanasheria Mkuu wa Serikali tunalipa kipaumbele” amesisitiza Wakili  Mkuu wa Serikali .

Amebainisha  kuwa  Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali  inatekeleza majukumu yake kwa niaba ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  hivyo  ni muhimu kwa Ofisi hizo kuwa na  mwelekeo na maono ya Pamoja  ili kuisaidia Serikali .

“Tunatekeleza  majukumu yetu kwa niaba yako Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali,    tunapaswa kuwa na maono na uelewa  wa Pamoja, tunapaswa kucheza kama  timu moja, hakuna mchezaji anayeweza kushinda bila ya  ushiriki wa wachezaji wengne ,  lengo letu si kushindana bali kuisaidia serikali   ishinde”  Akasema Wakili  Mkuu wa Serikali.

Aidha  katika mazungumzo hayo,  Ofisi hizo mbili pia zimekubaliana kuwatumia Mawakili  wa Serikali  waliomo  katika  Kanzi Data ya  Mawakili wa Serikali inayoratibiwa na  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  pale  watakapohitajika kuisaidia  serikali  kwa mijibu  wa  taaluma zao,  uwezo  na uzoefu wako  katika masuala  mbalimbali.

Octoba 10, 2022 Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliwateua Dkt. Boniface Christopher Luhende kuwa Wakili Mkuu wa Serikali  na alimteua Bi. Sara Duncan Mwaipopo kuwa Naibu Wakili  Mkuu wa Serikali.

mwisho