LONGOPA AMTAKA MKANDARASI MWANZA KUKAMILISHA MRADI KWA WAKATI

Na Mwandishi Wetu
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa amemtaka Mkandarasi anayejenga Jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoani Mwanza , kuhakikisha anajenga kwa viwango vinavyokubalika na kwa wakati.
Ametoa msisitizo huo siku ya Ijumaa wakati alipotembelea, kukagua na kuzungumza na Mkandarasi na kujionea kazi mbalimbali zinazoendelea katika eneo la mradi Buswero .
Akiwa katika eneo hilo, Dkt. Longopa pamoja na kumtaka mkandarasi kuzingatia viwango na muda wa mradi pia ameelezea kuridhishwa kwake na namna Mkandarasi huyo SUMAJKT alivyoanza kazi.
Katika maelezo yake kwa Naibu Mwanasheria Mkuu Dkt. Longopa, Mkandarasi pamoja na mambo mengine ameahidi kuukamilisha mradi huo kwa wakati ambao ni Miezi 18, kwa kuzingatia mkataba na kwa viwango.
Jengo OMMS mkoani Mwanza ni jengo ambalo ujenzi wake unagharamiwa na OMMS kwa gharama ya shilingi Bilioni Tatu hadi kukamilika kwake.
Aidha Jengo hili la Mwanza lenye ghorafa tatu (3)litakuwa Jengo la Kwanza la Kituo Jumuishi chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali litakalotumiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Ofisi ya Wakili Mkuu na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka
Baadhi ya kazi ambazo zimekwisha kuanza katika eneo hilo na ambalo Dkt Longopa alikuta vibarua wanaendelea na kazi ni pamoja na uchimbaji wa msingi.