MHAGAMA AWATAKA SUMA-JKT KUKAMILISHA MIRADI YA SERIKALI KWA WAKATI

Imewekwa: 08 May, 2023
MHAGAMA AWATAKA SUMA-JKT KUKAMILISHA MIRADI YA  SERIKALI KWA  WAKATI

MHAGAMA AWATAKA SUMA-JKT KUKAMILISHA MIRADI YA  SERIKALI KWA  WAKATI

Na Mwandishi Maalum

 

DODOMA- Waziri wa  Nchi Ofisi ya  Waziri Mkuu ( Sera, Bunge na Uratibu) Jenista  Mhagama (Mb) ameitaka Kampuni ya  Ujenzi  ya SUMA JKT kuhakikisha inatekeleza kwa wakati na kwa  ukamilifu  miradi ya ujenzi  ambayo  kampuni hiyo inapewa na  Serikali.

Akasema ni kwa kufanya hivyo ndipo ambapo Kampuni hiyo itaendelea kuaminiwa na Serikali na kupewa miradi  Zaidi  ya ujenzi.

Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki ( Jumamosi) wakati  alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la  Makao Makuu  ya  Ofisi ya Mwanasheria  Mkuu wa Serikali .  Jengo hilo  linajengwa  na Kampuni ya Ujenzi ya Suma JKT  katika Mji wa Serikali  Mtumba Mkoani Dodoma.

Akiwa katika  Mtaa wa Mwanasheria , mtaa ambao ndipo    linapojengwa   jengo hilo na  kupokelewa na Naibu Mwanasheria Mkuu  wa Serikali  Dkt. Evaristo Longopa,  Waziri Jenista Mhagama  alionyesha kutoridhishwa kwake  na kasi  ya   utekelezaji   wa mradi huo ambao kwa mujibu wa Mkandarasi na   Mshauri Muelekezi  mradi  ya  umefikia  asilimia 55 ya ujenzi  huku ukiwa   upo nyuma kwa  siku 60.

 Baada ya  kupokea taarifa hiyo fupi, Waziri Jenista Mhagama alisema. “Hapana   naona kuna shinda,  mkandarasi lazima  ujitathimini  na upitie upya ratiba ya utekelezaji wa mradi huu,  mpango wa serikali  nikuona  mradi wa ujenzi wa  Majengo ya Wizara na Taasisi  unakamilika  kabla ya  kufika tarehe 9/12/2023. Kwa maelezo yako Mhandisi  Muelekezi na Mkandarasi Napata shaka kama Jengo hili linaweza kukamilika kabla ya  mwezi desemba mwaka huu” akasema Mhe. Mhagama

 Na kuongeza  “ Suma JKT,  Serikali  inawapatia miradi mingi ya ujenzi siyo  tu huu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali  bali pia katika  maeneo tofauti tofauti  nchini, na inaonekana  kuna shida mahali miradi mingi haiendi kwa wakati, niwaombe sana  mujifanyie tathimini na kupitia tena ratiba za miradi yenu ukiwemo huu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ili  Pamoja na  mambo megine Serikali iendelee kuwaamini  na kuwapatia miradi  mingine.

Pamoja na  kuwataka SUMA JKT kujitathmini  Waziri Jenista Mhagama amesema Ofisi ya Mwanasheria  Mkuu wa Serikali  ni Ofisi  kubwa  ambayo inapaswa mambo yake Kwenda sawa kama ilivyo Ofisi yenyewe.

Na kwasababu hiyo ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kufuatilia  kwa karibu  utekelezaji wa   mradi huo  huku akisisitiza kwamba  jengo hilo  linatakiwa kukamilika  na kuanza kutumia kabla ya   Mwezi  Desemba  2023.

“Mhe. Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali  niwaombe sana  mfuatilie kwa karibu  utekelezaji wa mradi huu,  Ofisi hii ni kubwa, nitarudi tena  kufuatilia na kuona kama  maelekezo niliyotoa yamefanyiwa kazi. Mfuatilieni  mkandarasi kazi ambazo zinaweza kufanyika  kwa wakati mmoja bila shida ziendelee,  niwaombe sana pia mzingatie sana thamani ya  fedha  katika utekezaji wa mradi huu  na kubwa Zaidi nawatakia kila la kheri”. Akasema   Waziri  Mhagama.

Kwa  upande wake Naibu Mwanasheria Mkuu wa  Serikali Dkt. Evaristo  Longopa  akiwa ameambatana na watendaji  wengine kutoka Ofisi ya  Mwanasheria  Mkuu wa Serikali  alimshukuru Waziri Jenista Mhagama kwa  kutenga muda wake na kuutembelea na  kukagua maendeleo ya  ujenzi wa  Makao  Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Na akatumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya awamu na  Tano na  Sita kwa uthumbutu wa kujenga mji wa  serikali  mradi ambao  umechangia sana kubadilisha hadhi na taswira ya  Mkoa wa Dodoma

Dkt. Longopa amemhakikishia   Waziri  kuwa kwa kasi  inayoendelea hivi sasa ya umaliziaji  wa baadhi ya kazi  za ndani Pamoja na uwekezaji wa mifumo  mbalimbali   Jengo hilo linaweza kuanza kutumika kabla ya  mwezi  Desemba.

Aidha   Meneja wa SUMA JKT Kanda ya  Kati Meja Samule Jambo amemuhakikisha Mhe. Waziri kwamba jengo hilo  litakamilika kabla ya mwezi Desemba 2023.

Mradi wa ujenzi wa  Makao  Makuu  ya Ofisi ya  Mwanasheria  Mkuu wa  Serikali  hadi kukamilika kwake unatarajiwa kugharimu Tsh Bn 26.8.  matarajio ya mradi ni kukamilika kabla ya septemba 2023.

Pamoja na  kutembelea  Mradi wa Ujenzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali , Waziri Jenista Mhagama pia alitembelea na kukagua  eneo la ujenzi  Wizara ya  Utamaduni, Sanaa na  Michezo, Eneo la  Ujenzi wa Uwanja wa Mashujaa, Wizara ya  Maliasili na Utalii na Ofisi ya  Waziri Mkuu- Sera, Bunge na  Uratibu.

Imeandaliwa na  Kitengo  cha Mawasiliano

6/5/2023