PONGEZI TUNAZOPEWA ZIWE CHACHU KWETU-AG FELESHI

Imewekwa: 14 Jun, 2022
PONGEZI TUNAZOPEWA  ZIWE CHACHU KWETU-AG FELESHI

Na Mwandishi  wetu

14 June 2022

Kufuatia  pongezi nyingi  ambazo  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekuwa ikizipata,  huku nyingine zikitolewa mubashara.  Mhe. Jaji Dk. Eliezer Feleshi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amewaasa  watumishi wa Ofisi hiyo kuzitumia kama  chachu  ya kuendelea kufanya kazi kwa weledi, bidii, uadilifu, ubunifu na kwa wakati.

Ameyasema hayo  katika salamu zake za pongezi  kwa watumishi wa OMMS alizozitoa  kupitia   Naibu  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Dk. Evaristo Longopa ambapo  amemtaka  kuzifikisha pongezi hizo  kwa Watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

  Katika  salamu zake hizo, Mwanasheria  Mkuu wa Serikali  amesema,   pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili  Ofisi katika utekelezaji wa  majumuku yake, amekuwa akipokea salamu nyingi za pongezi  kutoka kwa wadau mbalimbali wanaopata  huduma zao kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali

“Pamoja na changamoto zinazoikabli Ofisi yetu ambazo tumeendelea kuzifanyia kazi kwa lengo la kuboresha zaidi  huduma zetu kwa wadau wetu,  hivi karibuni  Divisheni ya  Mikataba imeongeza sana kasi ya kushughulikia kazi zake kwa weledi na kwa wakati pamoja na  ukweli kwamba, mikataba mingine imekuwa ikiwasilishwa Ofisini kwetu kwa kuchelewa na ikiwa na mapungufu mengi” amesema AG

Amebainisha  kwamba,   mapema mwezi huu wa June,   alihudhuria  hafla  ambayo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu  Hassan   alikuwa anashuhudia utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa miradi ya  maji katika miji 28 iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino Dodoma.

“ Katika hafla hiyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ilipongezwa kwa dhati kwa jinsi  ilivyotekeleza majukumu  yake katika upekuzi wa mikataba husika kwa weledi  na kwa wakati licha ya baadhi ya mikataba hiyo kuwasilishwa kwa kuchelewa sana na ilitakiwa kutiwa saini ili kuruhusu hatua za utekelezaji kuanza” amesema AG.

Akizungumza katika hafla hiyo   Katibu Mkuu Wizara ya Maji Injinia  Anthony  Sanga alisema.

 “ Lakini  Mhe. Rais, naomba sana sana nisiache kumshukuru Mhe. Jaji Dk. Feleshi kwa kazi kubwa na  nzuri sana ambayo  ametusaidia Mwanasheria   wetu Mkuu wa Serikali,  mikataba mingine ilikwenda asubuhi na ikatoka jioni,kwa maana  imefanyiwa  upekuzi ndani ya siku  moja , tunamshukuru sana Jaji Feleshi”.

  AG Feleshi  amekwenda mbali  kwa  kubainisha  pia kwamba,  pamoja na  pongezi hizo zilizotolewa mubashara tarehe 6/6./2022 , amekuwa  akipokea mrejesho na pongezi za namna hiyo kutoka kwa wadau mbalimbali  kuhusiana na  huduma za kisheria zinazotolewa na  Divisheni ya Uandishi wa Sheria na Ile ya  Uratibu na Ushauri wa Sheria.

“ Kwa namna ya pekee, nimeona inafaa na ni jambo muhimu nikuletee ( DAG) ili ufikishe  pongezi hizi kwa  Mkurugenzi, Wakurugenzi Wasaidizi wa Divisheni ya Mikataba pamoja na Wakurugenzi, Wakurugenzi  Wasaidizi na watendaji wote wa Divisheni zingine  na kuwaomba waendelee kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu na kushughulikia kazi zinazotolewa  kwetu kwa wakati” amesisitiza Mhe. Feleshi.

Akaongeza kwa kusema. “ Naomba  pongezi hizi ziwe chachu kwa watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ya kuendelea kufanya kazi kwa weledi, bidii, uadilifu,  ubunifu na kwa wakati kwa maslahi ya  umma kwani  naamini kazi zetu zinatekelezwa kwa kupokezana  mfano  wa mnyororo ambapo kila afisa anayehusika kwa ngazi yake anachangia kutoa matokeo  chanya ya kazi zetu”.

Wakati huo huo, AG Feleshi  amesema , anapowasilisha pongezi hizi,  anawaomba  watumishi wote kuongeza kasi ya kukamilisha mpango wetu wa kutumia TEHAMA katika  kupokea, kuchakata na kuwasilisha matokeo ya kazi zetu kwa  wadau.

Mwisho.