TAASISI ZA FEDHA ZARIDHISHWA NA UTATUZI WA KERO ZAO

Imewekwa: 11 Aug, 2023
TAASISI  ZA FEDHA ZARIDHISHWA NA UTATUZI WA KERO ZAO

Na  Mwandishi Maalum

 

Dodoma-Imeelezwa kuwa vikao  kati ya  Serikali na  Wawakilishi  wa Benki na Taasisi za fedha vinavyoratibiwa na Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  vimeanza kuleta matokeo  Chanya.

 

Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa Benki ya CRDB Bw. Prosper Mwangamila wakati wa kikao kati ya  Serikali na  Umoja wa Benki Tanzania (Tanzania Banker’s Association-TBA) kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Mtumba, Dodoma. 

 

“Tunaishukuru   Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuandaa vikao hivi kwani vimeleta matokeo chanya ambapo kwa sasa mashauri yanayohusu benki  yamekuwa yakipewa kipaumbele” akasema Bw. Mwangamila.

 

Hata hivyo, pamoja na   kutoa shukrani hizo, Mwakilishi  huyo kutoka  CRDB  aliongeza kuwa bado zipo changamoto zinazotokana na rasilimali hasa katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.

 

Kikao hicho kilikuwa chini ya Uenyekiti wa Bw. Ipyana Mlilo,  Mkurugenzi  Msaidizi Sehemu ya  Uratibu, Divisheni ya Uratibu na Huduma za  Ushauri wa Kisheria (DCAS).

 

Akifungua  kikao hicho Bw. Ipyana Mlilo aliwaeleza wajumbe kuwa kikao hicho ni  muendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi ya kuwataka kukutana mara kwa mara ili  pamoja na  mambo mengine kuhakikisha  hatua mbalimbali  zinachukuliwa za kutatua changamoto  zinazoikabili Sekta ya  Fedha hapa nchini.

 

Kwa  mujibu wa Mwenyekiti wa Kikao Bw. Mlilo,  kikao hicho  cha Alhamisi tarehe 10 Agosti 2023, wajumbe  walijadiliana  kwa  kina changamoto na maazimio yaliyoazimiwa katika kikao  kilichofanyika  mwishoni  mwa  mwezi February 2023 Mkoani Dar es Salaam.

 

Akizungumzia  changamoto  zinazohusu Mabaraza ya  Ardhi na Nyumba ya Wilaya ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na  Benki na Taasisi za Fedha,  Mwakilishi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Hellen Phillip Njau, alikieleza kikao hicho kwamba,   Serikali  pamoja na  mambo mengine imendelea kuajiri watumishi wapya kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ili  kukabiliana na upungufu wa watumishi.

 

Akabinisha  kuwa,  Wizara imeendelea kutekeleza hatua kwa hatua baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika mabaraza hayo. Baadhi ya  maeneo ambayo yanamashauri  zaidi ya 400 wameongezwa  wenyeviti zaidi ya  mmoja na hivyo kupunguza tatizo la  ucheleweshaji wa mashauri.

 

 Naye  Mwakilishi  kutoka Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Bi. Antelma Mtemahanji  akielezea changamoto ya baadhi ya  Wakuu wa Mikoa na Wilaya  kujiwekea utaratibu wa kutoa vibali au  kuendesha majadiliano ya  ulipaji wa madeni nje ya  hukumu za mahakama,  na kwamba,  Katibu Mkuu OR- TAMISEMI  ameendelea kutoa maelekezo na miongozo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya  ya kutotakiwa kutoa vibali au kuingilia  suala la ulipaji wa madeni bali  wao wanapaswa  kupewa taarifa tu.

 

Kuhusu changamoto ya  urejeshwaii wa fedha zinazotokana na Majadiliano ya  Mashauri ya Jinai ( Plea Bargaining ) Mwakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya  Mashtaka   Bw.   Patrick Mwita ameeleza kuwa   baadhi ya  barua  zilizoandikwa  na  Benki   zilizokuwa na kesi za jinai  zimefika katika Ofisi hiyo  na Taasisi  zinazohusika zimejulishwa kwaajili ya malipo.

 

Aidha katika kutatua changamoto ya upotevu wa baadhi ya majalada ya mashauri ya ardhi  na Waheshimiwa  Mahakimu kuto ridhia matumizi ya nakala za mafaili  husika,   changamoto hiyo imeelezwa kuanza kufanyiwa kazi  kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na  Wizara ya Ardhi na Mahakama kwa kuunda   Mfumo  wa Mashauri  ( Intergrated Land Cases Management System (ILCMS) na kwamba mfumo huo upo katia hatua za majaribio.

 

Kwa kauli moja  wajumbe wa kikao hicho baada ya kujadili changamoto hizo, walikubaliana  kwamba, TBA wawasilishe changamoto hizo kwa Msajili wa Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI na kunakilishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili changamoto hizo ziweze kufanyiwa kazi.

 

Vile vile  katika kikao hicho  wajumbe  wamezishauri  Benki   kutoa taarifa muda wowote kwenye mamlaka hizo pindi wanapokutana na changamoto za kiutawala.

 

Kikao hicho kimehusisha pia Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  Msajili wa Hati, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Benki za Biashara ikiwemo CRDB,NMB na Equity.

 

Itakumbukwa  kuwa katika   Mkutano  Mkuu wa  Chama cha Mawakili  wa Serikali uliofanyika tarehe 29 Septemba, 2022, Mhe.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maekelezo kwa   Mwanasheria Mkuu wa Serikali yakumtaka akae na wawakilishi wa benki na taasisi za fedha ili kutatua changamoto zao ikiwemo ya mlundikano wa mashauri katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na Mahakamani.

 

mwisho

 

11/8/2023