TUMIENI VIZURI UPATIKAJAJI WA FEDHA KUKAMILISHA UJENZI- HAZINA

Imewekwa: 01 Jun, 2022
TUMIENI  VIZURI  UPATIKAJAJI WA FEDHA KUKAMILISHA  UJENZI- HAZINA

 

TUMIENI  VIZURI  UPATIKAJAJI WA FEDHA KUKAMILISHA  UJENZI- HAZINA

Na  Mwandishi  Wetu

Mtumba- Dodoma

01-06-2022

Wataalamu kutoka  Idara ya  Tathmini na  Ufuatiliaji wa Matumizi ya Fedha, Wizara ya  Fedha na Mipango, wamemshauri Mkandarasi ( SUMA JKT) anayejenga  jengo  jipya  la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba, kuhakikisha  anaitumia vema fursa ya  upatikanaji wa fedha za mradi  kutoka serikalini kwa  kuongeza kasi ya  utekelezaji wa kazi  za mradi.

Wametoa ushauri huo siku ya  Jumanne, wakati wataalamu  hao Bw.Elirehema Mollel na Bw. Lucipine Kahunduka wakiambatana na baadhi ya maafisa wa OMMS walipofika  eneo la ujenzi  kwa lengo la kupata taarifa za  ujenzi wa mradi huo pamoja,  kufahamu kama  fedha zinatolewa kwa wakati  na changamoto mbalimali zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi.

Kabla ya  kutembelea eneo la mradi wataalamu hao walikutana na  Kamati ya Ujenzi  ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali   ambapo walipatiwa taarifa ya  mradi   ikiwamo  taarifa ya  fedha ambazo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  imepatiwa kutoka Serikali Kuu, malipo  ambayo yamekwisha fanyika kwa mkandarani na mshauri mwelekezi  pamoja na changamoto zilizojitokeza  katika hatua za awali za maradi.

“ Katika  taarifa  mliyotupatia  inaonyesha mradi  upo nyuma  kwa  takribani  wiki  15 kutokana na sababu mbalimbali,  ingawa mmeongeza kasi  kupunguza pengo  hilo,  lakini ushauri wetu ni huu, tumieni  fursa hii ya mtiririko mzuri wa fedha  kutoka serikalini  kwa   kwa  kuongeza kasi ya  ujenzi   hata ikiwapasa kufanya kazi usiku na mchana  fanyeni  hivyo” akasema  Bw. Elirehema Mollel

Na kuongeza  “ kwa kufanya kazi usiku na mchana na kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi  ujenzi  utakwenda mbali na hata  kwa mfano,  pakitokea changamoto ya  upatikanaji wa fedha basi muwe mmeshapiga hatua kubwa au kufika mbali”.

Pamoja  na kumtaka mkandarasi huyo  kuongeza kasi, pia wamemshauri Mshauli mwelekezi   kutoka  Wakala wa Majengo ya Serikali  Bw. Peter  Muluki ,kuhakikisha  hakwamishi  kwa  namna yoyote ile ujenzi wa jengo hilo ambalo wataalamu wanasema, ni moja kati ya Majengo makubwa ya Serikali yanayoendelea kujengwa katika Mji wa Mtumba.

“ Tumeelezwa pia kwamba wewe (mshauri mwelekezi) pia  ulikuwa sababu ya kuchelewa kwa mradi huu kwa kuchelewa kutoa vibali au michoro, tungeomba  kwa hapa  ujenzi  ulipofikia   hatutegemei masuala ya  utoaji wa vibali au kubadilisha michoro  likajitokeza tena kwa sababu, pamoja na kuchelewesha ukamilishaji wa mradi  lakini pia kutaongeza gharama.

Na kwa sababu hiyo,Watalalamu  hao wameitaka OMMS, Mkandarasi na  Mshauri mwelekezi kuwa na  mawasiliano ya mara kwa mara ili kubaini  changamoto  na kuzitafutia  ufumbuzi wa haraka  na hivyo   kutokwamisha  mradi.

Akijibu  na kutoa ufafanuzi  wa hoja za wataalamu hao,  Meneja wa SUMA JKT kanda ya Kati Meja Samuel  Jambo aliwahikishiaka  wataalamu hao kwamba, pamoja na  kuwa  mradi huo umechelewa kwa wiki  15  lakini kasi wanayoendelea nayo sasa ni nzuri na kwamba, wanafanya kazi zaidi  ya moja  kwenye mradi bila kusubirisha.

Aidha, amesema  pamoja na  kuongeza muda  kwa kazi, lakini pia  wanazo malighafi za kutosha  kwa maana ya   Nondo,  Kokoto wanazotoka Tabora  na Cementi na    zitakidhi  mahitaji ya maradi kwa asilimia 40.

Na kuongeza kwamba  kwa kasi wanayokwenda nayo sasa na kama  hakutatokea  mabadiliko yoyote  mradi utakamilka  kwa wakati.

 Kwa upande wake, mshauri mwelekezi  Bwana Peter Muluki amesema, hategemei   kwa sasa  ujenzi ulipofikia kutokea mabadiliko makubwa ambayo yanaweza kupunguza kasi ya  utekelelezaji wa maradi huo au kuongeza gharama.

Akaahidi kutoa ushirikiano  kwa Mkandarasi ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu.

Naye Mkurugenzi wa Divisheni ya Mipango Bw. Buji Bampebuye akizungumza kwa niaba ya wajumbe wengine wa OMMS, amesema,  Ofisi imekuwa ikitekeleza wajibu wake kwa kuhakikisha kuwa mara inapo pata fedha kutoka  Hazina  inapeleka kwa mkandarasi kwa wakati.

Vile vile akabainisha Ofisi imekuwa na vikao vya mara  kwa mara vya kufanya  tathimini ya maendeleo ya  mradi na  vikao vya kitaalamu.

Jengo  jipya la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  linatarajiwa kugharimu  Tshs 26.817,046,474.13. Aidha  Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi September  2023.

Mwisho