VYAMA VYA USHIRIKA SEHEMU ZA KAZI VISAIDIE KUPUNGUZA CHANGAMOTO ZA WATUMISHI –AG FELESHI

Imewekwa: 16 Aug, 2022
VYAMA VYA USHIRIKA  SEHEMU ZA KAZI VISAIDIE KUPUNGUZA CHANGAMOTO ZA WATUMISHI –AG FELESHI

Na Mwandishi Maalum

16/8/2022

DODOMA

Mlezi wa  Chama cha Ushirika Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali “ SHERIA  SACCOS”  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Jaji Dk. Eliezer Feleshi amesema  kuanzishwa kwa  vyama vya ushirika maarufu kama Saccos sehemu za kazi kulilenga  katika kuwasaidia watumishi  kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwamo ulipaji  wa ada za watoto wao.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ameyasema hayo wakati alipokuwa akifungua   Mkutano  wa Wanachama  wa Sheria Saccos akiwa ni mlezi wa Chama hicho. Mkutano huo umefanyika  leo  Jumanne  katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ipagala Jijini Dodoma.

Katika Mkutano huo na ambao pia umehudhuriwa na Maafisa Ushirika kutoka Jiji la Dodoma, pamoja na  mambo mengine wanachama watafanya tathmini na  kujaidili changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili Saccos hiyo pamoja na kuweka mikakati madhubutu ya kuifufua tena na kuifanya iwe imara kama kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Kwanza, niwapongeze sana  kwa kufanya mkutano huu,   hii ilikuwa hamu yangu  ya muda mrefu  mkutane ili  pamoja na mambo mengine mjadiliane na kuweka mikakati madhubuti kuhusu  Saccos yetu. Nimefarijika sana” akasema Mwanasheria Mkuu  wa Serikali.

Mlezi  huyo wa Sheria Saccos amebainisha kuwa vyama vya ushirika  vilitiliwa mkazo sana na  Hayati Mwalimu Julius Nyerere na  baadaye Hayati Rais Benjamin Mkapa ambaye naye alihimiza sana kuwa, pamoja na  kipato  kinachotokana na mshahara, mtumishi awe na shughuli ya kujiingizia kipato kwa kujipatia mitaji kutoka Saccos hizo.

“Hakuna mtu anayependa kuishi maisha ya  shida, kila mtu anapenda kuishi kwa furaha. Vyama hivi vya ushirika  vitusaidie kuishi kwa furaha kwa kutusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwamo za kulipa karo za wanafunzi na mambo mengine. Kwa hiyo, kama mlezi ningependa kuona Saccos iliyo imara na inayosaidia kupata suluhu la changamoto za watumishi”. Akasema AG Feleshi.

Mlezi huyo wa Sheria Saccos amebainisha  pia kwamba katika  kuifanyia mageuzi makubwa Sheria Saccos  ni vema wanachama hao  kupitia mkutano  huo  wakajadiliana  pia namna ya kuvutia wanachama wapya ikiwani ni pamoja na kuwarejesha waliowahi kuwa wanachama.

Hata hivyo  amesisitiza kwamba,  ili kuwa na saccos imara na yenye kuwanufaisha wanachama ni  muhimu kuwa na viongozi na wanachama waadilifu.

“Nisisitize pia suala ya maadili kwa viongozi na wanachama,  ni  bora  mkabaki wachache waadilifu kuliko kuwa  na wanachama wengi wavurugaji.  Baadhi ya wanachama wanapokuja kuomba mkopo mikono inakuwa mbele wakishapata  mikopo  inakuwa shinda”.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia amebaisha kwamba licha ya changamoto ambayo Sheria Saccos imepitia,   bado  inabaki kuwa Saccos yenye  heshima kutokana  na  viongozi wengi wakiwamo  Wanasheria Wakuu wa Serikali waliopita, Wakurugenzi wa Mashtaka waliopita, wanasheria wengi na ambao wengine sasa ni majaji kuwa wanachama wa  Saccos hiyo.

 Akabinisha pia kuwa, akiwa  mlezi wa Sheria Saccos  itakuwa aibu sana kusikia kwenye   Sheria Saccos kuna ubadhirifu wa fedha na kwa sababu hiyo atasimima sana suala la uadilifu.

Aidha  amewataka Maafisa Ushirika kuwa   karibu na vyama vya Ushirika ili pamoja na mambo mengine kubaini mapema  changamoto na kuzitafutia ufumbuzi mapema.

Awali  Afisa Ushirika  Yusuf Timotoli akizungumza  wakati wa mkutano huo, amesema Sheria Saccos inakabiliwa na changamoto  kama ilivyo kwa Saccos nyingine nyingi zilizohamia Dodoma kutoka Dar es Salaam

Hata hivyo amesema Ofisi yao  imejitahidi kusaidia katika kuzifufua baadhi ya  Saccos ikiwamo ya Utumishi na sasa watahakikisha wanaisimamia kwa  karibu Sheria Saccos ili ifikie ubora wake.

Naye Mwenyekiti wa Sheria Saccos Bw. Richard Mbaruku amesema   Sheria Saccos ilikuwa na  Wanachama 91 lakini waliopo  sasa na ambao wapo hai ni 49. Wanachama wa Sheria Saccos ni wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,  Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali  na  Tume ya Kurekebisha Sheria.